1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Amstrong na kashfa ya madawa ya kuimarisha misuli

Kashfa ya bingwa mara saba wa mashindano ya mbio za baiskeli-Tour de France na kisa cha kufariki dunia watoto wachanga katika hospitali ya Charité mjini Berlin ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini .

Lance Amstrong akishangiria ushindi wake wa sabaa wa Tour de France mwaka 2005

Tuanzie lakini na kashfa inayoutikisa ulimwengu wa michezo na hasa mashindano ya mbio za baiskeli-Tour de France.Gazeti la "Schwarzwälder Bote" linahisi:"Yule ambae zamani alikuwa shujaa anaewika,hakuweza tena kutetewa-kwasababu hakuna tena anaeshuku kama kweli Amstrong ametumia madawa mengi kupita kiasi ya kuimarisha misuli.Ndio maana hukumu dhidi yake imekuwa kali sana.Lakini kibaya zaidi ni kwamba katika kesi hii kila mmoja ameondoka patupu-yeye mwenyewe-washindani wake "wanaojiita nadhifu" na bila ya shaka shirika la kimataifa la waendesha baiskeli-UCI ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifumbia macho yote mawili visa vya udanganyifu katika fani ya kuendesha baiskeli.Na ndio maana itakuwa kiroja mataji yote saba aliyopokonywa Lance Amstrong kuvikwa wengine-kwasababu na wao pia si nadhifu.

Lakini gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaandika hata hivyo:"Lance Amstrong bila ya shaka kuna wanaomsifu.Mfano anapoangaliwa kama mtu aliyepigana dhidi ya ugonjwa wa saratani-ugonjwa uliompata na ambao wengi wanauangalia kama mwisho wake ni mauti tu.Kwa kuunda wakfu wa kupambana na ugonjwa wa saratani,Amstrong amewapatia matumaini watu wengi walioshikwa na ugonjwa huo.Na mpaka katika wakati huu wa kiza kwake,watu wote hao bila ya shaka bado wanamuamini.Ni tukio lisilokuwa na mfano:Amstrong amepokonywa fulana zote saba za rangi ya njano-alizovikwa katika mashindano ya mbio za baiskeli ya Tour de France.Mmarekani huyo aliyedhibiti peke yake mashindano hayo kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2005,anajikuta uchi.Na shirika la kimataifa la mbio za baskeli ambalo jana limefuata muongozo wa shirika la mbio za baiskeli la Marekani na kumpokonya Amstrong mataji yote aliyovikwa katika mashindano ya Tour de France,linaonekana kana kwamba linazama katika janga la misukosuko.

Radrennen Pat McQuaid wa shirika la UCI akitangaza kupokonywa Amstrong mataji yake

Nalo gazeti la "Saarbrücker Zeitung "linasema:"Walimwengu wangebidi wagutuke tangu zamani.Mtu ambae George W. Bush amemtaja kuwa rafiki yake hawezi kuwa nadhifu.Hata shirika la kimataifa la mbio za baiskeli UCI hatimae limeungama na baada ya kufumba macho miaka nenda miaka rudi,limekiri kwamba Lance Amstrong ametumia baadhi ya wakati madawa ya kuimarisha misuli wakati wa enzi zake kama shujaa wa waendesha baiskeli.Lazma haikuwa rahisi kwao kukibwaga chini kitambulisho chao cha fahari.Seuze tena kwa miaka walikuwa waking'ara kileleni na kujifaharisha kuwa sehemu ya historia ya kusisimua ya mtu aliyeushinda nguvu ugonjwa wa saratani ,mtu aliyekipa kisogo kitanda cha mgonjwa na kupanda kileleni mwa fani ya kuendesha baaskeli."

Berlin Charité Campus Virchow-Klinikum

Mada ya mwisho magazetini inahusu kisa cha vijidudu vilivyosababisha kufariki watoto wachanga katika hospitali ya Charité mjini Berlin.Gazeti la "Berliner Morgenpost" linaandika"Kinachohuzunisha zaidi katika kisa cha kufariki dunia watoto wachanga na wengine waliozaliwa kabla ya wakati ni ule ukweli kwamba maradhi yao si majaaliwa ya Mungu bali yamesababishwa na mkono wa binaadamu.Na pengine hivyo hasa ndivyo ilikuwa.Kwasababu kama hakuna usafi-yaani kama watu hawakoshi mikono, basi hilo ni dhambi kubwa na sio tu katika hospitali za Ujerumani.Bado lakini chanzo cha vijidudu hivyo kinachunguzwa katika kituo cha watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati katika hospitali ya Campus Rudolf-Virchow-Klinikum.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu