1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 24.10.2012 | 15:37

Syria kuamua kuhusu pendekezo la Brahimi

Mjumbe wa amani kuhusu Syria Lakhdar Brahimi amesema leo kuwa serikali ya Syria imekubali kutekeleza pendekzo lake la usitishwaji wa muda mapigano wakati wa sherehe za kiislamu ya siku nne kuanzia Ijumaa. Hata hivyo Syria imesema kuwa jeshi lake bado linatathmini pendekezo hilo na uamuzi wa mwisho utatolewa kesho Alhamisi. Taarifa ya Syria iliziweka katika hali isiyoeleweka juhudi za Brahimi za kusitisha kwa muda, umwagikaji wa damu nchini humo, wakati waasi wanaopigana kumwondoa madarakani rais Bashar al Assad wakikosa kuonyesha dalili yoyote kuwa wako tayari kusitisha vita. Akizungumza katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo, Brahimi alisema kuwa baada ya ziara yake mjini Damascus, kuna makubaliano kutoka kwa serikali ya Syria ya kuweka chini silaha wakati wa siku kuu ya Eid. Lakini Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Syria imesema pendekezo hilo bado linajadiliwa na uongozi wa kijeshi. Wakati huo huo ndege za kivita za Syria zimefanya mashambulizi mengine ya angani katika mji ambao ni ngome ya waasi wa Maarat al Numan, huku waasi wakiizingira kambi moja ya kijeshi mashariki mwa mji huo. Watu watano kutoka familia moja, akiwemo mtoto na mwanamke mmoja waliuawa katika mashambulizi hayo ya angani.

Wanne wauawa katika mashambulizi ya Gaza

Hofu leo imetanda karibu na ukanda wa Gaza baada ya shambulizi la angani la Israel kuwauwa wanamgambo wanne, nayo makundi yenye silaha ya Kipalestina yakavurumisha zaidi ya maroketi 70 kusini mwa Israel, na kuwajeruhi vibaya watu wawili. Hilo ndilo ongezeko kubwa la ghasia za mipaka ya pande zote tangu mwezi juni, na kuilazimu Israel na makundi ya wanamgambo katika ukanda wa Gaza kuapa kuwa hawatakubali mashambulizi hayo kufanywa bila kujibiwa. Mashambulizi hayo ya hivi punde yalianza jana jioni, muda mfupi baada ya kukamilika ziara ya ngazi ya juu katika ukanda wa Gaza na Mfalme wa Qatar, wakati wanamgambo walipofyatua maroketi sita kusini mwa Israel. Israel kisha ikafanya mashambulizi mawili ya angani kaskazini mwa Gaza, na kuwauwa wanamgambo wawili kutoka kundi la Hamas, na kuwajeruhi watu wengine saba, na kuchochea mashambulizi mengine ya maroketi. Kufuatia machafuko hayo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak amefutilia mbali mazungumzo na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Mataifa aliyeko nchini humo Catherine Ashton, ili kuzuru eneo la mpakani la ukanda wa Gaza.

Moto katika kiwanda cha silaha Sudan

Sudan leo imeishutumu Israel kwa kukiripua kiwanda cha silaha na ikatishia kulipiza kisasi baada ya tukio hilo lililowauwa watu watatu. Waziri wa Utamaduni na Habari wa Sudan Ahmed Bilal Osman amesema leo kuwa wanadhani Israel ndiyo iliyohusika na mripuko huo. Amesema kuwa ndege nne zilihusika katika shambulizi hilo, lililotokea usiku katika kwianda cha silaha cha Yarmouk Kusini mwa Khartoum. Wakaazi wamesema ndege au kombora lilipiga juu ya kiwanda hicho muda mfupi kabla ya kuripuka na kuwaka moto. Awali, Gavana wa jimbo la Khartoum Abdulrahman al Khider alisema uchunguzi wa mwanzo umebainisha kuwa mripuko huo ulitokea katika ghala ya kuhifadhi silaha. Alipuuzilia mbali madai kwamba sababu nyingine zilisababisha tukio hilo. Khider amesema watu kadhaa wamelazwa hospitalini baada ya kupaliwa na moshi lakini hakuna aliyefariki.

Draghi apigia debe ununuzi wa hati za dhamana

Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi leo ameimarisha kampeni yake ya kutafuta uungaji mkono wa Ujerumani kuhusu mpango wa kukabiliana na mgogoro wa madeni katika benki hiyo, kwa kuwaambia wabunge mjini Berlin kuwa mpango wa benki hiyo wa kununua hati za  dhamana utasaidia kuondoa hofu kuhusu mgoro wa sarafu ya euro. Draghi ameuambia mkutano wa pamoja wa kamati tatu za Bunge la Ujerumani, kwamba mpango huo wa kununua hati za dhamana hautachochea ughali wa maisha wala kuhujumu uhuru wa benki kuu ya Ulaya. Aliongeza kuwa ununuzi wa hati za dhamana siyo hatua ya benki kuu ya Ulaya kusaidia kufadhili serikali za nchi wanachama, wala kusababisha athari nyingi kwa walipa kodi katika kanda ya sarafu ya euro. Mkutano huo wa Draghi, na wanachama wa kamati za fedha, bajeti na masuala ya Ulaya, ambao watahitajika kutathmini jibu la Ujerumani kwa mgogoro huo, ulifanywa faraghani. Mkuu huyo wa benki kuu ya Ulaya pia anatarajiwa kuulizwa maswali na wabunge kuhusu mgogoro wa kiuchumi unaoikumba Ugiriki.

Ugiriki kuongezewa muda wa kulipia mikopo

Ugiriki ambayo inakumbwa na mgogoro wa madeni imepewa muda zaidi na wadeni wake ili kutimiza malengo yake ya kifedha. Waziri wa fedha Yannis Stournaras ameyasema hayo bungeni leo muda mfupi baada ya kuwaambia waandishi wa habari kwamba ametia saini na wadeni wake kutoka Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuhusu muafaka mpya wa mpango wa kubana matumizi, ijapokuwa bado unahitaji kuidhinishwa na serikali ya muungano. Stournaras amesema ameukubali mpango wa kubana matumizi wa euro bilioni 13.5 ambao utasaidia kushughulikia mikopo iliyokwama ya Ugiriki. Duru kutoka Wizara ya fedha inasema rasimu mbili za sheria zinazohusiana na mpango huo zitawasilishwa bungeni wiki ijayo na kupigiwa kura Novemba mbili.

Kumbusho la wahanga wa Nazi lazinduliwa

Ujerumani leo imezindua kumbusho la kitaifa la mamia kwa maelfu ya Waroma na Wasinti waliouwawa wakati wa utawala wa Wanazi, huku Kansela Angela Merkel akisema kila kifo kilichotokea kinamsababishia maombolezo na aibu. Kumbusho hilo lililokuwa likisubiriwa tangu zamani limejengwa mfano wa hodhi lenye maji na mnara  ambao juu yake ua litakuwa likiwekwa kila siku. Kumbusho hilo linakutikana karibu na jengo la bunge katikati ya mji mkuu Berlin, na pia karibu na makumbusho mengine mawili ya wahanga wa ukatili wa wanazi: moja likiwa la wayahudi milioni sita na jengine dogo la mashoga. Wanahistoria wanakadiria kuwa kati ya Wasinti na Waroma 220,000 na 500,000 barani Ulaya waliuawa na wanazi, waliowachukulia kuwa tabaka la walio wachache.Kansela  Merkel aliungana na mamia ya manusura wa mauaji hayo ya halaiki wakiongozwa na kiongozi wa Baraza kuu la Wasinti na Waroma nchini Ujerumani, Romani Rose pamoja na rais Joachim Gauck.

Marekani na Umoja wa Ulaya zaonya kuhusu Lebanon

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeleezea wasiwasi wao kuhusu hali ya kisiasa nchini Lebanon, ambako upinzani umemtaka waziri mkuu ajiuzulu kuhusiana na mripuko mkubwa uliotokea nchini humo wiki iliyopita na kuinyooshea kidole cha lawama Syria. Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton ameonya dhidi ya pengo la kisiasa nchini Lebanon, wakati akikamilisha ziara yake nchini humo, akiunga mkono maoni kutoka Wizara ya Mambo ya kigeni ya Marekani.  Bibi Ashton pia alionya kuwa kuna baadhi ya watu wanaojaribu kuyageuza mawazo kutoka kwa hali halisi katika eneo hilo kwa kusababisha matatizo nchini Lebanon. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya kigeni ya Marekani Victoria Nuland  alisema Marekani inaunga mkono juhudi za Rais Michel Sleiman na viongozi wengine kuunda serikali madhubuti.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.de.